ad

ad

RC NDIKILO-VIGOGO WASIOJULIKANA WALIOVAMIA MSITU WA HIFADHI WA KAZIMZUMBWI WASAKWE

 
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo (Wa kwanza kushoto)na kaimu meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS)wilayani Kisarawe Mkoani Pwani, Endrew Mwenuo (wa pili kulia)na mkuu wa wilaya ya Kisarawe Happiness Seneda ( Wa kwanza kulia) wakiangalia namna uvamizi ulivyofanywa na baadhi ya watu na vigogo katika msitu wa Kazimzumbwi wilayani Kisarawe.
Kaimu meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS)wilayani Kisarawe Mkoani Pwani, Endrew Mwenuo (kushoto) akimwelekeza jambo mkuu wa Mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo kuhusiana na uvamizi uliofanywa na baadhi ya watu na vigogo katika msitu wa Kazimzumbwi.Picha na Mwamvua Mwinyi
VYOMBO vya ulinzi na usalama,Mkoani Pwani vimetakiwa kuwatafuta baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa ni vigogo,; kuvamia msitu wa Hifadhi wa Kazimzumbwi uliopo wilayani Kisarawe na kugawa viwanja.
 
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ,alitoa rai hiyo wakati alipotembelea msitu huo kujionea baadhi ya maeneo ambayo yalivamiwa na wavamizi hao.Alisema vigogo hao wamesababisha msitu huo kuingiliwa na kuvamiwa mara nne na kundi la watu ambao wanadai sehemu ya msitu ni mali yao. 
 
Mhandisi Ndikilo ,alieleza kundi hilo limekuwa likiisumbua serikali kwa kwenda mahakamani na kushindwa .Aidha alisema vyombo hivyo vifanye ufuatiliaji kujua ni vigogo gani ambao wamekuwa wakiwatumia baadhi ya watu kwenda kushtaki mahakamani ili wapewe maeneo hayo kwa ajili ya viwanja .
 
“Inadaiwa kuna kampuni ilikata viwanja zaidi ya 300 na kuwauzia watu jambo ambalo haliwezekani kwani msitu huo umehifadhiwa kisheria”alisema mhandisi Ndikilo.Mhandisi Ndikilo,alisema kuwa msitu huo ulindwe kwani ni kama mapafu ya kupumulia viwanda na hewa ukaa hivyo endapo msitu huo utaharibiwa itahatarisha afya za watu. 
 
“Serikali ya mkoa haikibali hili,nimeshangazwa na kusikia kuna tume imekuja hapa Kisarawe na kuwahoji wataalamu mbalimbali juu ya suala la msitu huu wakati hakuna rufaa ya kesi ambayo ilifunguliwa na wavamizi ambao walishindwa”:;
 
” Wakae wakijua tume hiyo mimi siitambui wala mkuu wa wilaya haitambui sababu haijatoa taarifa,” alisisitiza mhandisi Ndikilo.Mkuu huyo wa Mkoa alisema inawezekana kuna vigogo wanaofanya mipango hiyo ili waweze kupewa eneo hilo kwa ajili ya maslahi binafsi. 
 
Nae mkuu wa wilaya ya Kisarawe Happiness Seneda alisema, wavamizi hao wamekuwa wakiwatishia watakwenda kwa waziri mkuu hata kwa Rais Dk .John Magufuli kueleza wanaondolewa kwenye maeneo yao.
 
Awali akielezea juu ya uvamizi wa msitu huo kaimu meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilayani Kisarawe,Endrew Mwenuo alisema wavamizi hao wamefanya uharibifu mkubwa kwa kukata miti kwa ajili ya mbao, kuchoma mkaa na ukataji wa miti kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
 
Alieleza,wamekuwa wakifanya doria mara kwa mara lakini wavamizi hao wamekuwa wakiwatishia mgambo wanaofanya doria kwenye msitu huo.Mwenuo alisema,kumevunjwa vibanda na kuondolewa alama zilizowekwa na TFS ili kuondoa ushahidi wa eneo la msitu. 
 
Msitu wa Kazimzumbwi,una ukubwa wa hekta 4,862 ulitangazwa kuwa msitu wa hifadhi 1954.

No comments

Powered by Blogger.