ad

ad

WAZIRI WA NISHATI ARIDHISHWA NA KAZI YA UJENZI WA NJIA YA UMEME KUELEKEA STIEGLERS GORGE

 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( wa Nne kushoto) akikagua maeneo ambayo miundombinu ya usafirishaji umeme inajengwa kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100. Wa Tatu kulia ni Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo na wengine ni watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO wakati alipokuwa katika kijiji cha Dakawa mkoani Morogoro kukagua miundombinu ya usafirishaji umeme inayojengwa kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100.
Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100 ikiendelea. Kazi hiyo inatekelezwa na  kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO.
 
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha Umeme wa msongo wa kV 33 inayojengwa kuelekea eneo litakalotumika kuzalisha Umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).
 
Dkt. Kalemani aliyasema hayo mkoani Morogoro wakati alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa kazi ya maandalizi ya ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 2100 pamoja na kuzungumza na wananchi katika vijiji vinavyopitiwa na miundombinu hiyo ya kusafirisha Umeme.
 
Dkt. Kalemani alisema kuwa, maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa Umeme wa Stiegler’s yanajumuisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya Barabara na usafirishaji Umeme kuelekea eneo la Mradi ili mradi huo mkubwa utekelezwe kwa ufanisi. 
 
Alieleza kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo ya usafirishaji umeme unatekelezwa na kampuni ya ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO na kwamba miundombinu hiyo inajengwa kutoka katika kituo cha kituo cha kupoza umeme cha Msavu hadi Mto Rufiji ambapo ni takriban kilometa 170.
 
“Kwa Vijiji ambavyo vinapitiwa na mradi huu wa njia ya kusafirisha umeme, wananchi watafungiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kama ilivyo katika vijiji vingine vinavyopitiwa na miradi ya usambazaji umeme vijijini na hakuna fidia kwa wananchi watakaopisha miundombinu hii,” alisema Dkt Kalemani.
 
Alisema kuwa, mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Februari mwaka huu mara baada ya Mkandarasi kupatikana na kwamba ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kuelekea eneo hilo la mradi umetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 80 na utakamilika mwezi Aprili mwaka huu.
 
Meneja Mradi wa Stiegler’s Gorge kutoka TANESCO, Florence Gwang’ombe, alisema kuwa mradi huo wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme utaboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo ambayo hayakuwa na Umeme ikiwemo baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Morogoro, vijiji vya Matombo, Dakawa, Kisaki pamoja na kambi ya Maafisa wa Wanyamapori ya Matambwe.
 
Alisema kuwa, mradi unatarajiwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 6.1 hadi kukamilika kwake na kwamba nguzo zinazotumika katika mradi huo ni za miti na zege na katika sehemu nyingine umeme utasafirishwa kwa kutumia nyaya zitakazopitishwa ardhini.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alimpongeza Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya uamuzi wa kuanza kutekeleza mradi huo wa Stieglers Gorge ambao alisema kuwa utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini, utainua uchumi wa nchi kutokana na kuchochea uanzishwaji wa viwanda pamoja na maendeleo ya mtu mmoja mmoja kupitia shughuli mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme.

No comments

Powered by Blogger.