WALIOISHIA DARASA LA 7 NA WENYE VYETI FEKI HATIMA YAO KUJULIKANA MACHI MWAKA HUU
Hatma ya watumishi walioondolewa kazini na serikali kutokana na vyeti feki, itajulikana mwezi machi mwaka huu.
kauli hiyo imekuja baada ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), kukutana na baadhi ya viongozi wa serikali, akiwemo Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jehanista Muhagama, Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, george Mkuchika na Naibu waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Kakunda na kupeleka hoja 11 na kutatuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, jana, Katibu Mkuu wa TUCTA, Yahya Msigwa, alisema hatma ya watumishi hao, itajulikana mwezi Machi, mwaka huu, iwapo watalipwa fedha zao au la.
Msigwa alisema serikali inatambua kuwa watumishi hao wametenda kosa la jinai na la kinidhamu, lakini wataangalia jinsi watakavyoweza kuwacha.
“Baada ya kuishawishi serikali ili watu hao wasiondoke mikono mitupu, serikali ilisema bado mamlaka mbalimbali zinzohusika na masuala hayo, zinalifanyia kazi suala hilo,” alisema.
Aliongeza “Serikali imesema huenda kabla ya Machi hadi Aprili, mwaka huu, kabla ya sherehe za Mei Mosi, itajulikana hatma yao, kama wanaweza kuondoka na kitu kidogo kwa sababu kimsingi tunaendelea kuipigia serikali goti ili kuwafikiria.”
Hoja nyingine, iliyojadiliwa ni kuhusiana na ajira kwa walioishia darasa la saba, ambapo serikali iliahidi kuwalipa na kuwarudisha kazini baadhi yao, ifikapo Machi, mwaka huu.
“Taasisi mbalimbali zimetakiwa kufanya tathmini dhidi ya watu wa darasa la saba ili kuona hali ikoje na Ofisi ya Katibu Mkuu TUCTA, ikishirikiana na Ofisi ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, kuratibu suala hilo,” alisema.
Akizungumzia upandishaji madaraja, alisema lilishindikana kutokana na zoezi la uhakiki wa wafanyakazi wenye vyeti feki.
Msigwa alisema kutokana na kukamilika kw azoezi la uhakiki, serikali itawapandisha madaraja na baadhi yao tayari walishapandishwa.
“Tulijadiliana kuhusu madeni ya wafanyakazi, serikali ikasema lazima yahakikiwe ili kuweza kulipwa na yatahakikiwa kwa sababu mengi watu waliyoyapeleka siyo sahihi,” alisema.
Aliongeza kuwa, serikali imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya ulipaji huo na wanzazisubiri ili wafanyakazi waweze kuondokana na hali ngumu ya maisha.
Kuhusu nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi, Msigwa alisema haikuwa ahadi ya serikali kwa mwaka uliopita, bali kila mmoja alikuwa akipewa kiinua mgongo.
Alifafanua kuwa , Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aliahidi kuwaongeza Mshahara mwaka huu na hakuna barua ya mfanyakazi iliyoandikwa kuongezewa, hivyo alitaka kuacha kulalamika bila sababu.
Post a Comment